Halmashauri ya Mji wa Bunda kupitia Idara ya Elimu Sekondari leo imefanya hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Kidato cha Nne na Sita mwaka 2022.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Anney ambaye alikuwa mgeni rasmi amewapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri na kuwasaa kutobweteka na ufaulu walioupata.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amesema anatambua juhudi na jitihada za walimu na ndio maana anawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mgeni Rasmi ameeleza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanafunzi wote wanafaulu na kuendelea na masomo ya juu, kwa kufanya hivyo itapunguza pia kasi ya udokozi na wizi katika maeneo yetu unaofanywa na watoto waliofeli na kukosa kazi ya kufanya.
Dkt. Anney amewaasa wanafunzi kuendelea kujisomea kwa bidii ili waweze kujenga kesho yao iliyo nzuri. Aidha, Dokta ameahidi kwa siku zijazo kuwa ataanda hafla nyingine ya kuwapatia motisha walimu ili waendelee kufanya vizuri.
Manthalani, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amewataka walimu hasa wa masomo ya sayansi kuwa wabunifu katika ufundishaji wao ili kufanya masomo kuonekana rahisi kwa wanafunzi. Lakini pia amesema ni muhimu kuwapa motisha walimu ili kuwa na moyo wa kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bwn. Emmanuel Mkongo alieleza dhana ya Serikali kuboresha Sekta ya Elimu ya Sekondari hasa kwa kuboresha miundombinu ya Elimu kwa kuleta fedha za ujenzi wa madarasa na maabara za sayansi ambapo kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda shule zote za Serikali zimepata miradi hiyo.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda