"Mikopo mliyopewa ni fedha za Umma, ni fedha za watu walipa Kodi, ni fedha za watoa Ushuru wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, nasi kwa kufuata Sheria, na Maelekezo ya Serikali tumetenga 10% kwaajili ya kutoa Mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Wengi wanazitaka hizi fedha lakini ninyi mmepata bahati ya kuzipata kwaiyo mpanaswa mkazifanyie kazi ili muweze kurejesha kwa wakati ili tuwapatie watu wengine nao waweze kunufaika na mkopo huu".
Hayo yamesemwa na Mhe. Joshua Nassari, Mkuu wa Wilaya ya Bunda leo tarehe 13/12/2021 alipokuwa Mgeni Rasmi katika Hafla fupi ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mhe. Nassari ameeleza kuwa atafuatilia vikundi vyote vitakavyokaidi kuleta marejesho kwani kutorejesha ni kuvunja Sheria za Nchi. Ameeleza zaidi kuwa baada ya miezi miwili atatembelea vikundi vyote vilivyopewa mkopo kuona maendeleo yao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mhe. Michael Kweka amemshukuru Mgeni Rasmi kwa kutoa muda wake kuja kukabidhi mikopo hii kwa niaba ya Halmashauri. Aidha, ameviasa vikundi kutumia fedha hizo kwa malengo kusudiwa ya kikundi na si vinginevyo "kama ni biashara zikatumike katika biashara na kama ni kilimo basi ikatumike ipasavyo" Mhe. Kweka amesisitiza. Hata hivyo, Mheshimiwa Mwenyekiti amevikumbusha vikundi kufanya marejesho hasa vikundi vya vijana ambavyo vimejijengea tabia ya kutorejesha.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda ndugu Emmanuel Mkongo, ameeleza kuwa fedha hizi zimetokana na asilimia 10% ya Makusanyo ya ndani ya Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kipindi cha Robo ya kwanza Julai – Septemba 2021. Mkongo amevishauri vikundi hivyo kutumia fedha hizi vizuri ili ziwanufaishe kimaisha.
Awali Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Bonji Bugeni alitoa taarifa kuwa Jumla ya vikundi 17 vitapata mkopo huu kwa mchanganuo wa vikundi 9 vya Wanawake, 6 vya Vijana na Viwili vya Watu Wenye Ulemavu.
Halmashauri ya Mji wa Bunda imetoa jumla ya shilingi Milioni Hamsini kwa vikundi 17 vya Wajasilimali Wadogo.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda