Mkutano wa kawaida wa Baraza la Halmashauri ya Mji wa Bunda limekaa leo kueleza shughuli za utekelezaji robo ya pili 2022/23.
Kamati nne za Halmashauri ya Mji wa Bunda ambazo ni Kamati ya Fedha, Kamati ya Mipango Miji, Kamati ya Elimu, Afya na Uchumi pamoja na Kamati ya UKIMWI kupitia kwa Wenyeviti wa Kamati ziliwasilisha taarifa ya utekelezaji robo ya pili na wajumbe kupata fursa ya kutoa maoni yao.
Aidha, Taasisi ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), Wakala wa Barabara Mjini na Vijini (TARURA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nao walipata nafasi ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji robo ya pili katika eneo la Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Kupitia Baraza hilo, wajumbe walijadiliana na kukubaliana kuhusu suala la mlima Kaswaka kwamba wataalam walifanyie kazi haraka na kuwasilisha mapendekezo katika vikao vya kisheria.
Wajumbe walitaka kufahamishwa juu ya mradi wa kulima barabara unaofanywa na walengwa wa TASAF kama ni mpango wa Halmashauri ya Mji wa Bunda au wa Kitaifa ambapo majibu yalitolewa kwamba mpango huo ni wa Kitaifa ulioletwa na TASAF ikiwa na lengo la kuwakumbusha walengwa kwamba wanatakiwa kujishughulisha na kazi mbalimbali zinazoweza kuwaingizia kipato na si kukaa tu kusubiri fedha za kunusuru kaya masikini. Zaidi elimu iendelee kutolewa ili Walengwa walio na mitazamo hasi juu ya mradi huo waelewe malengo ya mradi. Aidha Uongozi umekili kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika kumetokea changamoto za kuchelewa kwa vifaa jambo lilipopelekea walengwa wengi kutumia vifaa vyao.
Baraza limeeleza pia suala la kuchelewa kwa fidia ya Wananchi walioharibiwa mazao yao na Tembo kwamba suala hilo lilishafikishwa katika Wizara husika na sasa kinachofanyika ni kuandika barua za kukumbusha na pindi yatakapokua tayari basi wananchi hao watalipwa.
Baraza kupitia kwa Mkurugenzi Emmanuel Mkongo limeeleza kuwa kupitia manunuzi ya jumla (Bulk procurement) katika ujenzi wa madarasa ya Sekondari kwa mwaka huu imeweza kuoka kiasi cha fedha ambacho kitawasilishwa katika Kamati ya fedha kwaajili ya kupangiwa matumizi na kuelekezwa kwenye Sekondari zenye changamoto.
Aidha katika upande wa Mamlaka ya barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kupitia kwa Mwakilishi wa meneja wa TARURA Mhandisi Michael amesema bajeti iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni Bilioni 2.09 ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kukarabati na kutengeneza barabara zote zilizomo kwenye bajeti. Mhandisi Michael amewatoa hofu Waheshimiwa Madiwani kwamba barabara zote zitafanyiwa kazi na zile ambazo hazimo kwenye bajeti hii zimezingatiwa katika bajeti ijayo 2023/2024.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bi. Esther Gilyoma amesema kwa Mwaka huu walikua na miradi kadhaa ambayo walikua wanaitekeleza na kuimalizia. Miradi hiyo ni mradi wa Chujio la Maji Nyabehu ambao umefikia 99%, Mradi za Tenki la maji Misisi Zanzibar ambao tayari Wananchi wameshanza kutumia maji na miradi mingine ambayo wanatarajia kumalizia mwaka huu wa fedha ni mradi wa Manyamanyama Mgaja na Balili Kunzugu.
Aidha, Mkurugenzi ameongeza kusema kuwa wanatarajia kutekeleza miradi mikubwa ya Sehemu ya kuhifadhi majitaka eneo la Butakale, na pia wanatarajia kujenga tenki la cubic meter 400 katika mlima Kilimahewa na miradi mingine mingi.
Katika wasilisho la Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limesema miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa mwaka huu ni mradi wa Kilimahewa Maralindi ambapo tayari umeme unawaka, Mradi wa Manyamanyama Mbugani, Mradi wa Rwabu, Mradi wa Kilimahewa Juu. Katika miradi hiyo kilichobaki ni waya ili kukamilisha mradi.
Kuhusu mradi wa REA tayari mitaa yote isiyo na umeme imeshawasilishwa kwaajili ya kuwekwa kwenye bajeti.
Mwisho Baraza limetoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Kaimu Mkurugenzi wa Malmaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira, pamoja na Meneja TARURA kwa kazi nzuri wanazofanya katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda