Adeladius Makwega-Musoma MARA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amempokea rasmi Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Aswege Enock Kaminyoge aliyefika kurepoti leo baada ya kuhamishiwa akitokea Wilaya ya Maswa na kumtaka kusimamia amani na utulivu na hususan mwaka huu wa uchaguzi Mkuu.
Mhe. Mtambi amesema wakati wa uchaguzi wako baadhi ya watu wanapenda kuanzisha chochochoko na kuongeza kuwa Mkoa wa Mara hautaruhusu mtu yoyote aichezee amani na utulivu uliopo kwa sasa.
“Shabaha yetu ni kujenga uchumi wa Mkoa na hususani kwa ajili ya wananchi wanaoishi katika Mkoa wa Mara ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa na hayo yatafanikiwa tu endapo amani na utulivu vitaendelea kutawala” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mara kuwa makini na homa za kisiasa zinazoweza kuvuruga amani na utulivu uliopo na kuutoa Mkoa kwenye adhma yake ya kukuza uchumi wa wananchi wake.
Kanali Mtambi amewataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wananchi wapo salama na wanaendelea kufanya shughuli zao kama kawaida na wanasiasa wanafanya siasa zao kama kawaida kwa amani na utulivu kwa kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.
“Pale Bunda Mji tuna madini na wananchi wapo kazini wakichimba madini yaliyogundulika katika eneo hilo na wajibu wetu kama Serikali ni kuwawekea mazingira wachimbaji hao wadogo waweze kufanya shughuli zao na kulipa kodi zinazohitajika kwa Serikali” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumza katika mapokezi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe.Kaminyoge amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini.
Mhe. Kaminyonge amesema atatekeleza maagizo aliyompatia kwa nguvu na moyo wote na kuwaomba wananchi wa Wilaya ya Bunda kumpokea na kumpatia ushirikiano.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vincent Naano Anney amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi kwa kufanya naye kazi vizuri kwa kipindi chote akiwa Bunda na kuahidi kufanya kazi kwa vizuri akiwa Maswa kwa maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda