Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia mradi wa TACTIC imesema Halmashauri ya Mji wa Bunda ni miongoni mwa Halmashauri 45 zitakazo nufaika na Mradi wa TACTIC (Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness) kuboresha baadhi ya maeneo yenye kutoa huduma kwa wananchi kwa kiasi kikubwa ili kupunguza changamoto zinazotokana na kukua kwa Miji na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi.
Miradi iliyopendekezwa na Halmashauri kupitia Wadau na Wananchi ni Stendi Kuu, Soko Kuu, Barabara za Kiwango cha lami Kilometa 25.3, Ujenzi wa Dampo la kisasa, Egesho la Malori na Machinjio ya Kisasa.
Hayo yamesemwa katika Kikao cha Wataalamu kutoka OR-TAMISEMI na Viongozi wa Halmashauri pamoja na Wadau wa Maendeleo wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, kilichofanyika tarehe 16/12/2021 siku ya Ijumaa.
Katika Kikao hicho, Mhandisi kutoka TAMISEMI ndugu Rashid Mtamila amesema hii ni moja ya juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha huduma kwa wananchi. Mhandisi ameeleza kuwa mradi huu ni muendelezo wa Miradi iliyopita ya TSP na ULGSP katika kuboresha Miundombinu ya Miji Tanzania.
Kwa upande wa Mazingira, Ndugu Kivuyo kupitia Mpango Mkakati wa Masuala ya Kimazingira (SESA) amesema kazi yao kubwa ni kuandaa miongozo (Mpango kazi) itakayosimamia mradi huu wa TACTIC kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mradi. Aidha, ameeleza zaidi kuwa Mpango unalenga kuangalia athari za kimazingira zitokanazo na utekelezaji wa mradi na pia kutoa elimu na kupata maoni kutoka kwa Wananchi juu ya athari za Kimazingira na kuzitatua.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mhe. Michael Kweka amesema Halmashauri ya Mji wa Bunda ipo tayari kupokea mradi huu na jambo jema ni kwamba maeneo yote yaliyopendekezwa hayahitaji fidia yoyote kwa wananchi kwani ni maeneo ya Halmashauri. Pia, Mheshimiwa Mwenyekiti ameiomba TAMISEMI kuingalia Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa jicho la kipekee kupewa kipaumbele katika kutekeleza mradi huu.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndugu Emmanuel Mkongo, amesema utekelezaji wa mradi huo utachagizwa mpango na ndoto za Halmashauri kuwa Manispaa na kuufanya Mji wa Bunda kukua kwa kasi Zaidi. Ameeleza zaidi kuwa Wakazi na Watendaji wote wa Halmashauri ya Mji wapo tayari kupokea mradi na wanatamani kuona mradi huu ukianza kutekelezwa.
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa mradi umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza linashirikisha Halmashauri 12, kundi la pili Halmashauri 15, na kundi la mwisho Halmashauri 18. Katika awamu ya kwanza Benki ya Dunia inategemewa kutoa Dola za Kimarekani Milioni 500.
Mradi unatarajiwa kuanza mwezi Julai 2022 kwa Halmashauri za kundi la kwanza na baada ya miezi sita makundi yaliyosalia yataanza kutekeleza mradi huo.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda