Tarehe 04.01.2023
Ziara ya Mawaziri nane wa Kisekta wakiongozwa na Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mheshimiwa Angelina Mabula imefika Kata ya Nyatwali iliyopo Halmashauri ya Mji wa Bunda kuwaeleza wananchi msimamo wa Serikali kulitwaa eneo la Nyatwali (Ghuba ya Speke) kuliunganisha na hifadhi ya Serengeti.
Serikali imesema inatwaa eneo hilo kwa manufaa makubwa ya Taifa na Usalama wa Wananchi wa Nyatwali dhidi ya Wanyama wakali wa porini.
Aidha, Mawaziri hao wamewaondoa hofu Wananchi wa Nyatwali juu ya stahiki zao na mahali ambapo watakwenda mara baada ya kuhamishwa. Wasema Serikali imejipanga kuhakikisha kule ambako Wananchi watahamia huduma zote za msingi kama ambavyo zilikua zinapatikana katika eneo hilo la Nyatwali zitapatikana kama kawaida.
Huduma za afya, Elimu, ufugaji, Kilimo na umwagiliaji, huduma ya maji vyote vitazingatiwa.
Aidha mheshimiwa Mabula amesema Serikali haitawabeba na kuwapeleka sehemu fulani na badala yake baada ya uthamini na malipo kufanyika Serikali itawaelekeza maeneo ambayo yametengwa ambayo mwananchi atachagua wapi ahamie, yaweza kuwa ndani ya mkoa wa mara au nje ya mkoa.
Mheshimiwa Mabula amewatoa hofu Wananchi hao juu ya mwekezaji katika eneo hilo na kusema, hakuna mwekezaji ambae anakuja kulichukua eneo hilo, hayo ni maneno ya uongo na uzushi na yapuuzwe.
Aidha mheshimiwa Mabula amewaomba Wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea na zoezi la uthamini na kila mwananchi atalipwa kulingana na sheria, taratibu na kanuni za nchi bila kumuonea mtu hata mmoja. Gharama za uthamini wa vitu tayari wananchi walishaelezwa na zimebandikwa katika mbao za matangazo.
Awali Wizara zote nane za Kisekta zilizieleza jinsi gani zilivyojipanga kuhakikisha haki na huduma stahiki kwa Wananchi hao zinazingatiwa popote pale watakapokwenda.
Kabla ya Mkutano wa Hadhara, kilifanyika kikao cha ndani cha Mawaziri na Uongozi wa mkoa na Wilaya ya Bunda ambapo mheshimiwa Joshua Nassari Mkuu wa Wilaya alieleza hatua mbalimbali zilizofanyika kuanzia mwanzo hadi sasa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kuanza zoezi la uthamini.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda