“Nimefika hapa Bunda Mji niwapongeze kwa kazi nzuri ambazo mnaendelea nazo za ujenzi wa Madarasa. Madarasa ukiyaona yanaviwango, tofali zimenyoka ziko vizuri unaona kabisa kuna ushirikiano mkubwa wa mafundi katika kazi na nimeambiwa kwamba tofali hizi mnafyatua wenyewe kwenye kiwanda cha Halmashauri jambo ambalo ni ubunifu mzuri wa kuongeza mapato ya Halmashauri. Lazima Halmashauri nyingine zijifunze kupitia Halmashauri hizi.”
Hayo yamesemwa na Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo J. Dugange wakati akitembelea na kukagua ujenzi wa madarasa 59 unaoendelea ndani ya Halmashauri ya Mji wa Bunda. Mheshimiwa Waziri amesema lengo la ziara hii ni kushirikiana, kushauriana na kupeana mawazo ya namna ya kutekeleza ujenzi wa miradi ya elimu, afya na miradi mingine ambayo ina dhumuni la kuboresha huduma za jamii na kuwezesha wanafunzi wa Sekondari na shule za Msingi katika kujifunza katika mazingira bora.
Mheshimiwa Naibu Waziri ameongeza kwa kusema kuwa miradi hii inatakiwa kukamilika tarehe 30/12/2021 licha ya changamoto za vitendea kazi zilizojitokeza ambazo zilikua ni za nchi nzima. "Jambo la Msingi Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi mjipange kuongeza nguvukazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi huu kama mlivyokubaliana kukabidhi kwa RAS tarehe 27/12/2021." Amesisitiza Mheshimiwa Dugange.
Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais ameleta fedha nyingi sana akiwa na imani na watu wanaozisimamia. Amisitiza kuwa Mwezi Januari kutakuwa na chaguo moja tu la wanafunzi na wote watatakiwa kuingia darasani.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Ndg. Albert Msovela amemweleza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba jambo la KIPEKEE na la utofauti katika ujenzi uliofanywa na Halmashauri ya Mji wa Bunda ni kwamba wameweka vigae madarasani na kujenga Ofisi za Walimu katikati ya madarasa hayo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Joshua Nassari amemueleza Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa kitu ambacho kimechelewesha kasi ya ujenzi huu ni upatikanaji wa saruji, jambo ambalo aliamua kulivalia njuga kwenda Tanga kiwandani na kufanikisha kulipia mifuko ya saruji elfu kumi na saba (17,000) na kusafirisha kutoka Tanga hadi Bunda ili kukabiliana na Changamoto ya Saruji hususani katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yenye miradi mingi ikiwemo ya Ujenzi wa Vituo vya Afya, Hospitali ya Wilaya, Jengo la huduma za dharura, Madarasa na ujenzi wa Jengo la Ofisi za Halmashauri. Hata hivyo, Mheshimiwa Nassari amesema kwa sasa ujenzi huu utaenda kasi kwasababu uwepo wa saruji ya kutosha.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndg. Emmanuel Mkongo amemuomba Mheshimiwa Naibu Waziri kusaidia kutatua shida ya Maji katika shule ya Sekondari Bunda ambayo ni shule ya bweni wasichana na Wavulana kwa kidato cha tano na sita, ambapo Mheshimiwa Naibu Waziri amelichukua kwa utekelezaji Zaidi.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda