Mradi wa Kilimo Hifadhi kutoka Kanisa la AICT Dayosis ya Mara na Ukerewe imetoa mafunzo kwa Maafisa Kilimo kata na Wakulima Wawezeshaji 55 kutoka Halmashauri ya Mji Bunda, Serengeti na Butiama kuhusiana na Mbinu shirikishi/jumuishi za udhibiti wa wadudu waharibifu na matumizi sahihi ya viuatilifu.
Akizungumza katika mafunzo hayo Afisa Mradi wa Kilimo Hifadhi Bw. Charles Loleku amesema baada ya mafunzo haya wanategemea washiriki kwenda kuwafundisha Wakulima wengine katika maeneo yao ili kufanya Kilimo chenye tija.
"Mafunzo haya tumefanya kwa siku tatu na baada ya hapo zoezi litakua endelevu kwenda kuwafundisha Wakulima kwasababu tunataka mpaka Wakulima wanapofikia msimu basi wawe na Uelewa wa kutosha kabla ya uvamizi wa wadudu." Amesema Charles Loleku.
Bwana Loleku ameongeza kusema "bila Chakula hatuwezi kufanya kazi yoyote kwahiyo sisi tuna haki na wajibu wa kuhakikisha usalama wa Chakula katika maeneo yetu tunayofanya kazi."
Kwa upande wake Afisa Kilimo Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Adelina Mfikwa amesema anayofuraha kwa mafunzo haya kufanyika katika Halmashauri yake na jumla ya washiriki kutoka Halmashauri ya Mji wa Bunda ni Maafisa Kilimo 13 na Wakulima Wawezeshaji 7.
Bi. Adelina amesema "AICT wamekua wadau wetu wakubwa kwenye kutekeleza Kilimo Hifadhi na kutokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi Wakulima hawanabudi kupata hii teknolojia ya Kilimo Hifadhi Ili uzalishaji wa mazao usitetereke kwa kiasi kikubwa na mahali pengine tuboreshe Afya ya udongo tuweze kuongeza uzalishaji."
Aidha Bi. Adelina amesema kuwa matarajio yetu ni kwamba Maafisa Kilimo na Wakulima Wawezeshaji waliofundishwa watapeleka Elimu sahihi kwa maeneo wanayotoka ili kuongeza uzalishaji wa Chakula.
Hata Hivyo Afisa Kilimo hakusita kutoa rai kwa Wakulima kuchukua tahadhari ya usalama pindi wanapotumia viuatilifu na wazingatie maelekezo husika ya viuatilifu kwa kusoma vibandiko vilivyopo kwenye chupa za viuatilifu ambavyo vimeandikwa kwa lugha rafiki ya Kiswahili.
Mradi wa Kilimo Hifadhi ni Mradi wa AICT Dayosis ya Mara na Ukerewe unaofanya kazi kwa kushirikiana na Serikali wenye lengo la kuboresha Afya ya udongo ili kuweza kuongeza uzalishaji.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda