Baraza la Halmashauri ya Mji wa Bunda chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Michael Kweka limekubali na kupitisha mpango na bajeti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wenye thamani ya shilingi Bilioni 32,923,527,000/-
Baraza limeeleza kuwa Bajeti hiyo imezingatia vipaumbele vya Halmashauri ikiwemo, mishahara ya Watumishi, miradi ya Maendeleo pamoja na shughuli mbalimbali zinazojitokeza hatika Halmashauri ikiwemo uendeshaji wa Halmashauri.
Waheshimiwa Madiwani wameahidi kuilinda bajeti hiyo, ili iweze kutekelezwa kama ilivyokusudiwa katika kila idara na Halmashauri kwa ujumla.
Aidha katika baraza hilo, wajumbe walitaka kujua kwa kina kuhusiana na suala la miradi ya TASAF ya ulimaji barabara jinsi ilivyopangwa ambapo walielezwa kwamba miradi hiyo inatekelezwa chini miongozo iliyoletwa na TASAF Makao Makuu na sio kwamba inapangwa na Halmashauri.
Hata hivyo Halmashauri imekiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mradi huo ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi kama vile majembe, gloves pamoja na sululu.
Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg. Emmanuel Mkongo amekiri kuzipokea changamoto hizo na kuziwasilisha katika Mamlaka husika.
Awali, Waheshimiwa Madiwani waliwasilisha mapendekezo ya bajeti ya kufanya ziara ya kujifunza katika Halmashauri nyingine ambapo majibu yalitolewa na Mkurugenzi kwamba suala ni jema japokua linakwamishwa na ufinyu wa mapato ya Halmashauri.
Na pia Waheshimiwa Madiwani wameitaka Halmashauri kuwashirikisha katika miradi yote ya maendeleo ambayo inaelekezwa katani. Katika hilo Mkurugenzi Mkongo alisema tayari suala hilo lilishafanyiwa kazi na maelekezo yalishatolewa kwa watendaji wa kata kutoa taarifa ya miradi yote inayotekelezwa katani iwe miradi ya Elimu, Afya au miradi mingineyo.
Mwisho Baraza la Halmashauri limepitisha viwango vya ushuru wa huduma kwa wafanyabiashara wasiokuwa na hesabu za biashara wanaopaswa kulipa ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 kwa mujibu wa Sheria.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda