Mkutano wa Baraza la Halmashauri ya Mji wa Bunda chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Michael Kweka limeketi leo kupitia na kujadili punguzo la bei ya Viwanja kwaajili ya wananchi wa Kata ya Nyatwali wanaohama kupisha eneo hilo kuwa sehemu ya Hifadhi ya wanyama ya Serengeti.
Akitoa ufafanuzi wa ajenda hiyo Mkurugenzi Bwn. Juma Haji Juma amesema Halmashauri imefikia hatua hiyo katika kuteleleza agizo la Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mara la kutafuta Viwanja ambavyo wananchi wa Nyatwali wenye malengo ya kuendelea kuishi katika Halmashauri ya Mji wa Bunda wapate viwanja kwa bei nafuu.
Mkurugenzi ameeleza kuwa mchakato wa kupunguza bei ulianza katika Vikao vya Menejimenti na Kisha kupitishwa katika Kamati ya Fedha na mwisho kuletwa katika Baraza.
Baada ya Ufafanuzi huo wajumbe walipitia na kutoa maoni yao na kisha kuridhia mapendekezo hayo na kuyapitisha. Aidha Baraza limeitaka Mejimenti katika Vikao vijavyo kuandaa taarifa inayoonesha fidia hasa kwa upande wa mali za Serikali zilizopo katika Kata hiyo.
Na pia Baraza limeielekeza Menejimenti katika Baraza lijalo kualika Uongozi wa TANAPA ili kuweza kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali ya Waheshimiwa Madiwani jinsi hali itakavyokua hasa baada ya Wananchi wa Nyatwali kuhama.
Awali Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Bwn. Salum Mtelela wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kikao alisema Serikali wakati inaanzisha mchakato huu ilihusisha Baraza la Madiwani na kufanya Vikao mbalimbali kujadili suala hilo ikiwemo Baraza Maalum kujadili kuhamishwa kwa wakazi wa Kata ya Nyatwali.
Akimalizia kujibu hoja, Katibu Tawala amewataka Waheshimiwa Madiwani kufika Ofisini kwake kueleza jambo lolote linalohitaji utatuzi wa haraka kuliko kusubiri Vikao.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda