Leo Jumapili limefanyika Bonanza Kubwa la michezo lenye lengo la kuelimisha na Kuhamasisha SENSA kwa Wananchi wa Kata ya Kibara na maeneo jirani.
Mgeni rasmi katika bonanza hilo Mheshimiwa Joshua Nassari Mkuu wa Wilaya ya Bunda ametoa rai kwa Wananchi wote wa Bunda kujiandaa kuhesabiwa ifikapo tarehe 23.08.2022.
Mheshimiwa Nassari ameongeza kusema kuwa "Sensa ya mwaka 2012 takwimu zinaonesha kuwa Bunda tulifanya vizuri sana hivyo Mwaka huu tujiandae kufanya vizuri zaidi" Aidha amewaasa Wananchi kutoa Taarifa sahihi kwa makarani pindi watakapofika kukusanya taarifa katika nyumba zao.
Naye Diwani wa Kata ya Kibara Mheshimiwa Mtamwega Mgayiwa, amesema zoezi hili la Sensa halina Chama sio la Chadema wala CCM ni zoezi la Kitaifa hivyo Wananchi wote mjitokeze kwa wingi kuhesabiwa ifikapo tarehe 23.08.2022. Mheshimiwa Diwani ameongeza kusema kuwa linapokuja suala la Kitaifa Wananchi wote tunapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambae pia ni Afisa Maendeleo Bwana Noel Shamazugu amewashukuru na kuwapongeza wakazi wa Kibara kwa kujitokeza kwa wingi katika bonanza na kuwaomba kujitokeza kwa wingi siku ya kuhesabiwa.
Awali Kijana mzalendo alieandaa zoezi hili ambae ni Mwenyekiti wa Vyama vya siasa Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla Ndugu Godwin Misana amesema wameandaa Bonanza hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda mahususi kabisa kufikisha Elimu ya Sensa kwa Wananchi wa Kata ya Kibara Ili kuwaweka tayari kuhesabiwa itakapofika tarehe 23.08.2022.
Aidha amewaomba Vijana wenzake wa Kata ya Kibara kuhakikisha wanaunga Mkongo juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta Maendeleo ya kweli katika Kata yao na Taifa kwa ujumla.
Mwisho Viongozi wa Serikali ya mtaa pamoja na Wananchi wa Kibara wamefurahishwa na ujio wa bonanza hilo na wamesema kuwa wapo tayari kuhesabiwa.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda