Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini imetoa msaada wa chakula (mahindi) kwa wahanga wa mafuriko katika Kata ya Nyatwali zaidi ya magunia 24 ili kuwapunguzia wananchi makali ya athari za mafuriko.
Akizungumza kabla ya kukabidhi chakula hicho, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Anney amewapa pole wakazi wa Nyatwali waliokumbwa na janga hilo na amesema Serikali inatambua matatizo yanayowakabili wananyatwali na ndio maana inafanya jitihada kuona namna gani itaweza kuwasaidia wananchi wake.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amesema, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Maeneo mbalimbali ya Nchi, mafuriko yametokea sehemu nyingi sana ndani ya Tanzania ikiwemo kata Nyatwali lakini pamoja na hayo Serikali haijawaacha wananchi wake kuhakikisha wanakua salama.
Akijibu swali la wananchi kuomba Serikali kuharakisha zoezi la kuwahamisha katika eneo hilo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amesema Serikali ipo katika hatua ya mwisho kukamilisha fidia za kuhama na pindi utaratibu utakapokamilika basi itawahamisha mara moja.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge Bwn. Emmanuel ametoa salamu za pole kutoka kwa Mheshimiwa Maboto na kusema kuwa Mheshimiwa Mbunge anatambua hali wanayopitia wahanga wa mafuriko hayo ikiwa ni pamoja na kuharibikiwa kwa chakula na mazao yao na ndio maana ameguswa kuchangia chakula japo kwa Uchache ili kiweze kuwasaidia wananchi wake.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Adelina Mfikwa amesema Halmashauri inaendelea kufanya tathimini ya janga hilo kupata idadi kamili ya wahanga ili iweze kutoa huduma ya makavelo yatakayoweza kuwasaidia kujistili kwa muda lakini pia Bi. Mfikwa amesema Halmashauri itatafuta chakula na kuwasilisha kwa wahanga kadri kitakapopatikana.
Hadi kufikia sasa takwimu zinaonesha zaidi ya kaya 160 zimeathiriwa na mafuriko katika Kata ya Nyatwali.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda