Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Vicent Anney amempongeza Ndg. Joseph Juma Keraryo kwa kuweza kuikumbuka shule yake ya Msingi na kuweza kurudisha fadhila kwa kutoa mashine ya kutolea kopi, Kompyuta, Rimu na kufanya sherehe ya pamoja na walimu na kutoa zawadi kwa kila mwalimu.
Mkuu wa Wilaya amesema Joseph ameunga mkono juhudi zinazofanywa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha Elimu. Aidha, Dkt. Anney ameutaka uongozi wa shule hiyo kuvitumia vizuri vifaa hivyo ili viwe chachu ya kuinua taaluma katika shule hiyo kwa kutoa machapisho ya mitihani na mazoezi mbalimbali.
Mheshimiwa DC amewataka wanabunda kuiga mfano mzuri Joseph kurudisha fadhila katika shule zao walizosoma.
Kwa upande wake Mkurugeni wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bwn. Emmanuel Mkongo amesema Joseph Keraryo ametoa funzo kwa wengi kukumbuka kule walikotoka na kunukuu maneno aliyowahi kusema Hayati baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere kwamba "Usijiulize Tanzania imekufanyia nini bali jiulize kwamba umeifanyia nini Tanzana". Akiwa na maana ya ni wajibu wetu sisi kama Watanzania kuijenga nchi yetu kama alivyofanya Bwn. Joseph Keraryo kuikumbuka shule yake.
Awali Bwn. Joseph Keraryo alisema ameamua kufanya hayo ili kuongeza nguvu katika kuwaandaa wanafunzi wa shule yake ya zamani ili kuhakikisha ufaulu unapanda kwa kasi katika shule hiyo.
Joseph amesema ametumia zaidi ya shilingi milioni sita kuhakikisha anafanya jambo katika shule yake aliyohitimu darasa la saba mwaka 2011.
Mwisho amewashauri vijana wenzake kuacha alama nzuri katika maeneo wanayoishi, wanayofanya kazi, wanakoabudu au katika shule walizosoma ili kuunga mkono juhudu zinazofanywa na Serikali kuleta Maendeleo nchini.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda