Ijumaa, 04.08.2023
Kikao cha kwanza cha Bodi ya Afya ya Halmashauri ya Mji wa Bunda chini ya Mwenyekiti Dkt. Pius Tubeti kimekaa leo kupitia taarifa ya utekelezaji ya Idara ya Afya kwa kipindi cha mwaka Mzima 2022/2023.
Idara iliwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa upande wa Idara nzima ya Afya, Kitengo cha Lishe na Ustawi wa Jamii.
Bodi imepongeza jitihada mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na idara ya Afya kuhakikisha Sekta ya Afya inakua bora na kutoa huduma bora kwa jamii.
Aidha, Bodi imetoa ushauri kwa Idara kufanyia kazi baadhi ya mambo ili kuboresha zaidi huduma ya afya. Baadhi ya mambo waliyoshauri ni kuongeza jitihada katika kutoa Elimu kwa jamii kuzingatia Lishe bora kwa watoto na watu wazima ili kuepuka utapiamlo.
Bodi imetoa ushauri kwa idara ya afya kwa kushirikiana na wajumbe wa bodi kuongeza hamasa kwa wanaume na wanawake kujitokeza kwa wingi kupima Afya ili hatua stahiki za matibabu zianze kuchukuliwa kwa watakaobainika kuwa na changamoto za kiafya kama virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine.
Bodi pia imetoa ushauri kwa kitengo cha Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wajumbe wa bodi wote kwa pamoja kuendelea kuelimisha jamii juu ya Ukatili wa kijinsia, malezi bora kwa watoto na wazee na kuhamasisha amani katika familia ili kuepusha migogoro isiyo na tija na inayoharibu ustawi wa familia.
Kikao kimekua chenye mafanikio makubwa sana na Bodi imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Idara ya Afya kuhakikisha wanaboresha sekta ya Afya katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda