OFISI ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji wa Bunda, imekabidhi kilogramu Elfu moja (1000) za unga wa mahindi kwa kaya zilizokumbwa na maafa ya mafuriko kata ya Nyatwali. Akikabidhi mifuko hiyo ya Unga Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mheshimiwa Mayaya Magesse ametoa pole kwa familia zote zilizopata maafa ya mafuriko na kuwapongeza wadau wote wanaojitokeza kutoa misaada kwa wahanga. Amesema, Serikali ipo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu cha mpito. Aidha ametoa wito kwa wadau wote wanaotoa misaada kutoingiza itikadi za vyama vya siasa badala yake walenge kuwasaidia wahanga hao.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Janeth Mayanja amesema kuwa misaada inayokuja itumike kwa malengo yaliyokusudiwa. Kamati inayohusika na ugawaji, ihakikishe walengwa wote wananufaika na misaada hiyo na sio kufanya udhalimu wa aina yoyote.
Hata ivyo ametoa wito kwa wakazi wote wanaoishi katika maeneo hatarishi ya mafuriko, kuondoka haraka katika maeneo hayo kwasababu majanga haya ya mafuriko huwa yanajirudia, leo tumepata athari ya kupoteza mali kesho keshokutwa athari inaweza kuwa kubwa zaidi hata kupoteza uhai.
Pia amewakumbusha wananchi kuendelea kujikinga na Ugonjwa wa homa ya mapafu COVID – 19 kwa kufuata tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa Afya. Hayo yote yamefanyika katika Ofisi ya Kata ya Nyatwali ambayo ndio kituo cha ugawaji wa misaada kwa wahanga hao wa mafuriko.
Jumla ya nyumba 178 zimebomoka, 133 zimeingiliwa maji na mashamba takribani 188 yameharibiwa na maji.
Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mahusiano
Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda