HALMASHAURI ya Mji wa Bunda imeadhimisha siku ya wanawake duniani katika kituo cha watoto yatima cha ST. FRANCIS WA ASSIZ kilichopo kata ya Kunzugu leo tarehe 07/03/2021. Maadhimisho haya yameambatana na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto kama unga mchele, sabuni za kufulia, juice, sukari, madaftari, kalamu, mafuta ya kupaka na ya kupikia na vitu vingine vingi.
Mgeni rasmi katika tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lydia Simion Bupilipili ameipongeza Halmashauriya Mji wa Bunda kwa kuwathamini watoto yatima na wenye mazingira magumu kwa kuchagua kuadhimisha tukio hili katika kituo hiki. Amesema kitendo hiki kitatambulisha kituo kwa watu wengi zaidi maana wengi walikua hawakifahamu. Hivyo amewaomba wananchi wote kujitokeza kwa wingi kuwasaidia watoto hawa kwa chochote wanachobarikiwa.
Aidha mgeni rasmi, amewataka wanawake kujitambua na kujielewa, kuamka na kuchakarika na kujihusisha na shughuli mbalimbali zitakazowaingizia kipato na sio kubweteka, kukaa kusubiri mwanaume awatimizie kila kitu.
Kwa upande wa viongozi, Mheshimiwa mgeni rasmi amewataka viongozi wanawake kuwatumikia wananchi kwa haki na usawa kwa wote ili kuifikia dunia yenye usawa.
Mwenyekitiwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ndugu Michael Kweka, ameushukuru uongozi wa kituo cha watoto Yatima kukubali kufanyia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika kituo hiki. Aidha amewaomba wakazi wa mji wa bunda kuwa mabarozi kwa watu wote kujitoa kwa moyo kukisaidia kituo hiki.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Janet Mayanja alieleza jinsi wananchi walivyoguswa kuwachangia watoto yatima katika maadhimisho haya. Amesema kuwa “makundi mbalimbali yamejitokeza kuleta zawadi kwa watoto akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, viongozi mbalimbali wa Vyama, Taasisi na Serikali na vikundi mbalimbali vya kijasiliamali.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, amewaomba sana wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kuwasomesha watoto wao ili kuwaandaa kuwa viongozi wa baadae. Na pia amewapongeza wanawake ambao wamejiunga na vikundi vya Vicoba na kuwajulisha kwamba sasaivi Wizara ya fedha kwa kushirikiana na benki kuu imeandaa utaratibu wa kuvitambua na kuvirasimisha vikundi vyote vya Vicoba. Hii itasaidia vikundi vingi kukopesheka katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa urahisi.
Aidha, Wageni mbalimbali waliakwa kushiriki maadhimisho haya na baadhi yao walitoa salamu kwa wanawake waliojitokeza kwa wingi kusherehekea siku ya wanawake Duniani.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Bunda alitoa neno kwa kusema “Wanawake ni jeshi kubwa na sisi tuliozaliwa na mwanamke tunamthamini sana mwanamke kwamba ndie mkombozi na Kila mwanaume aliefanikiwa basi kuna mwanamke nyuma yake”
Naye mwakilishi kutoka ofisi ya TANAPA kanda ya Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii Bi. Neema Philipo Mollel, Amewahamasisha wanawake wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kufanya utalii katika hifadhi bora kuliko zote Afrika, hifadhi ya Serengeti iliyopo katika mazingira yetu. Amesema “TANAPA imeandaa ofa ya kwenda kutalii kwa makundi kwa kutumia usafiri wa basi kwa gharama nafuu ya shilingi elfu Arobaini inayojumlisha gharama za usafiri wa kwenda na kurudi pamoja na chakula. Ofa hii itaendelea hadi sikukuu ya Pasaka.
Kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani kwa mwaka 2021 inasema, : Wanawake katika Uongozi: Chachu kufikia dunia yenye usawa.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda