LEO tarehe 15/12/2020, Jumla ya waheshimiwa madiwani 19 wa Halmashauri ya Mji wa Bunda wametoa kiapo chao cha kuidhinishwa Udiwani na kiapo cha uadilifu wa Umma mbele ya Mheshimiwa hakimu Husna Msangi wa Mahakama ya mwanzo na mbele ya Afisa wa Tume ya Maadili ya Mkoa wa Mara.
Baada ya kiapo hicho, Waheshimiwa Madiwa walipewa rasmi mamlaka ya kuwatumikia wananchi katika kata zao ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo na kutatua kero zilizopo katika maeneo yao. Hata hivyo waheshimiwa madiwani walipewa nafasi ya kufanya Uchaguzi ambapo Ndugu Kweka M. Thomas, diwani wa kata ya Sazira amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na Ndugu Mathayo Juma diwani wa Kata ya Manyamanyama kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Akiongea katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bi. Lydia Simion Bupilili amewapongeza sana waheshimiwa madiwani kwa ushindi mkubwa walioupata katika Uchaguzi na kuwaomba kushirikiana vyema na Wataalamu wa Halmashuri kuhakikisha shughuli zote za maendeleo zinatekelezwa ipasavyo. Pia amewaomba waheshimiwa madiwani kuainisha mitaa yao kwa kuweka vibao vinavyoonesha majina ya mitaa hiyo.
Awali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda ambae alikua mwenyekiti wa muda wa kikao hicho kabla ya kuchaguliwa Mwenyekiti wa Madiwani, Mheshimiwa Salum Halifan Mtellela amewaomba na kuwasisitiza waheshimiwa Madiwa kuhakikisha maendeleo yanapatika katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na kusema kuwa maendeleo haya yatapatikana ikiwa mtafanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu. Ameongeza pia, kazi kubwa iliyopo mbele kwa sasa ni kuhakikisha maboma ya madarasa yanakamilika, madawati yanapatikana na mwezi January, 2021 wanafunzi waingie shuleni.
Nae ndugu Method Nkoba, Mkuu wa Serikali za mitaa Mkoa wa Mara, amewasisitiza sana waheshimiwa Madiwani kuhakikisha shughuli zote za msingi zinafanyika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuhakikisha vikao vyote vya mitaa vinafanyika na kuandika Mihtasari ya vikao hivyo.
Mwisho, Mkurugenzi wa Halmashuri ya Mji wa Bunda ambae ndie Katibu wa baraza la madiwani Bi. Janeth Mayanja, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kipindi cha mwezi wa 7 mwaka 2020 lilipovunjwa baraza la madiwani hadi kufikia sasa. Waheshimiwa madiwani waliipokea taarifa hiyo na kuelewesheshwa pale walipohitaji kueleweshwa.
Halmashauri ya Mji wa Bunda inajumla ya Madiwani 14 waliochaguliwa kulingana na idadi ya kata na madiwani watano wa Viti Maalumu. Jumla wanakuwa madiwani 19 katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda