Zaidi ya shilingi milioni 58 za mfuko wa jimbo la Bunda mjini kwa Mwaka wa fedha 2022/2023 zimetumika kutengeneza madawati 1049 ya shule za Msingi ili kukabiliana na upungufu wa madawati uliopo sasa.
Mheshimiwa Robert C. Maboto Mbunge wa jimbo kwa Bunda mjini amesema kupitia Kamati ya mfuko wa jimbo na Baraza la Halmashauri kwa pamoja waliamua fedha zote za mfuko wa jimbo kwa Mwaka huu kutumika kutengeneza madawati kutokana na changamoto hiyo kuwa kubwa.
Aidha, Mheshimiwa Maboto amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za mfuko wa jimbo ambazo zinatumika kuleta maendeleo katika jimbo la Bunda mjini pia amelishukuru Baraza la Halmashauri ya Mji wa Bunda pamoja na watalamu wakiongozwa na Mkurugenzi kwa kumkubalia kuzielekeza fedha hizo katika kutengeneza madawati.
Mheshimiwa Maboto amesema yapo baadhi ya majimbo hayanufaiki na Fedha za mfuko wa jimbo na wala wananchi wake hawajui zinakokwenda na hakuna wa kuhoji, lakini kwa upande wake amesema jambo hili ni tofauti kwani Fedha zote za mfuko wa jimbo zinawekwa mezani na kupangiwa matumizi kadili ya mahitaji mbalimbali ndani ya jimbo.
Maboto amesema kama tutaenda kwa mwendo huu, tutaona tofauti kubwa sana katika jimbo letu la Bunda Mjini. Miradi itaonekana na thamani ya Fedha inayoletwa na Serikali itaonekana.
Aidha, Mheshimiwa Michael Kweka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kwaniaba ya Halmashauri kwa ujumla amemshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kukubali pendekezo la matumizi ya fedha hiyo kutengeneza madawati. Mwenyekiti amesema Mheshimiwa Maboto anaonesha mfano mzuri wa kuwajali wananchi wake kwa vitendo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Emmanuel Mkongo amesema Halmashauri kupitia mapato ya ndani imejipanga pia kutengeneza madawati mengine ya shule ya Msingi kwa Mwaka ujao ili kuendelea kupunguza upungufu wa madawati. Aidha, ametumia fursa hiyo kuwajulisha wananchi kwamba Serikali imeleta fedha zaidi shilingi Bilioni moja kupitia mradi wa BOOST kwaajili ya Ujenzi wa shule za msingi mbili mpya, Ujenzi wa madarasa 16 na matundu ya vyoo 24 katika shule za Msingi. Mwisho amewaomba wananchi kulinda mali za Serikali kwa faida ya vizazi vyao.
#kaziiendelee
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda