Kwa takribani wiki moja na siku kadhaa kuanzia tarehe 28/12/2020 hadi tarehe 05/01/2021, Mheshimiwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Janeth P. Mayanja amefanya ziara ya kutembelea na kuhamasisha maendeleo ya ujenzi wa shule sita mpya za sekondari zinazojengwa kwa nguvu ya wananchi katika kata za Bunda stoo, Mcharo, Nyamakokoto, Manyamanyama na Nyatwali.
Mheshimiwa Mkurugenzi ameonesha kuridhishwa na ujenzi unaoendelea katika shule hizo na kuzipongeza kamati za ujenzi kwa usimamizi mzuri wa michango ya wanachi katika ujenzi huo. Amesema “Mwananchi akiona michango anayotoa inafanya kazi iliyokusudiwa anakuwa na moyo wa kuendelea kushiriki katika michango na shughuli mbalimbali za mandeleo katika kata yake”.
Aidha ametoa wito kwa watendaji wa kata kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi kila mara inapoitajika ili waweze kujua ni jinsi gani michango yao inafanya kazi.
Kutokana maendeleo ya ujenzi wa Sekondari hizo, Mkurugenzi amesema jumla ya shule nne kati ya sita zinazojengwa zitasajiliwa na kufunguliwa mwezi Januari, 2021 ili kukidhi mahitaji ya watoto waliofaulu na kukosa nafasi katika shule zilizopo. Shule zitakazo funguliwa Januari hii ni shule inayojengwa Kata ya Mcharo, Kata ya Nyatwali na shule mbili ambazo zipo kata ya Bunda stoo, moja ikiwa mtaa wa Idara ya Maji na nyingine ikiwa Mtaa wa Migungani. Tayali hatua za usajili zimeshaanza kuchukuliwa.
Halmashauri ya Mji wa Bunda haikuwa mbali kushiriki katika ujenzi huo, Mheshimiwa Mkurugenzi alieleza michango iliyotolewa na Ofisi katika shule hizo ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa vyoo vyote kwa sekondari zinazojengwa.
Wawakilishi wa wananchi wa Kata, Waheshimwa madiwani akiwepo Mh. Flaviani Nyamageko Diwani wa kata ya Bunda Stoo, Mheshimiwa Mhigi Samson Sharya Diwani wa kata ya Mcharo, Mheshimiwa Juma Mathayo Machiru Diwani wa kata ya Manyamanyama, Mheshimiwa Emmanuel Machumu Maligwa Diwani wa Kata ya Nyamakokoto na Mheshimiwa Malongo Mashimo Diwani wa Kata ya Nyatwali, Wamempongeza Mkurugenzi kwa kazi kubwa anayoifanya katika kata zao kuhakikisha shule hizi zinakamilika na kumuahidi ukamilishaji wa ujenzi huo kwa wakati. Aidha waheshimiwa Madiwani wamewahakikishia wananchi wao kwamba kuanzia sasa hakuna udanganyifu wala pesa yoyote ile wanayochanga kupotea. Wamesema pia wapo tayali kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo ya kata kwa ujumla.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda