Leo umefanyika Mkutano wa Baraza la Halmashauri chini ya Mwenyekiti wa Baraza Mheshimiwa Michael Kweka. Mkutano ulianza kwa maswali ya papo kwa papo ambapo Mwenyekiti alitoa nafasi kwa waheshimiwa Madiwani kuuliza maswali mbalimbali ili kupata ufafanuzi na kujibiwa na Mkurugenzi Bwn. Emmanuel Mkongo.
Kupitia Mkutano huo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Dkt. Vicent Anney alipata fursa ya kuhutubia Baraza ambapo alianza kwa kutoa pongezi kwa Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi lakini pia alitoa msisitizo katika mambo mbalimbali ikiwemo utatuzi wa migogoro ya wananchi hasa migogoro ya ardhi na kuitaka mamlaka husika kuanzia ngazi ya mtaa kushughulikia migogoro hiyo. Pia baraza kuwa makini katika ununuzi wa vifaa na kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato kwani kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa mapato hasa kwa mabasi yanayobeba abiria na mizigo.
Aidha mkuu wa wilaya aliendelea kwa kusisitiza usafi wa mazingira na kuzitaka idara husika na TARURA kuwa makini katika kuzingatia usafi wa mitaro inayopitisha maji. Pia ofisi ya mazingira kuhakikisha wamiliki wa maduka na baa wanakuwa na dustbin za kutunzia taka za aina mbalimbali ili kutenganisha aina za taka, na kwa wale wote watakaoenda kinyume watozwe faini.
Mkuu wa wilaya alimalizia kwa kuwataka Madiwani kusimamia nidhamu ya watumishi hasa watendaji wa ngazi za chini mitaa na kata kwani hawakai katika vituo vyao vya kazi. Na kuwasihi kuheshimu muda wa kazi.
Baraza lilitoa pongezi kwa Mhandisi Baraka kwa kuhakikisha miradi ya utengenezaji wa barabara inakwenda vizuri na kumsihi kuendelea kusimamia miradi iende vizuri zaidi.
Mwenyekiti wa baraza alimalizia kwa kuwaomba wajumbe wote kuendelea kushikamana, kuchapa kazi na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Halmashauri ya Mji wa Bunda inaendelea kufanya vizuri katika kuwatumikia wananchi.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda