Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi. Janeth P. Mayanja ambae ndie Mgeni Rasmi wa uzinduzi huu, amezindua rasmi semina ya Uchaguzi kwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata (ARO – KATA) leo tarehe 07/08/2020 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Akizungumza na washiriki wa semina hiyo, Mgeni rasmi Bi Janeth P. Mayanja amesema, “Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 74 kifungu cha 6, Tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani. Hata hivyo pamoja na kuwa tume ndio yenye jukumu hilo, watakao simamia uchaguzi huu katika Mikoa na Halmashauri kwa ukaribu ni nyinyi tuliowateua na watendaji wa vituo watakaoteuliwa siku za mbeleni”.
Mgeni rasmi ameongezea kwa kusema kuwa Uchaguzi ni mchakato ambao unajumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazofuatwa na kuzingatiwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Maelekezo ya tume. Kwa kuzingatia na kutekeleza taratibu hizo kutapunguza au kuondoa kabisa kabisa malalamiko au vurugu wakati wowote wa uchaguzi.
Aidha, amewataka wateule hao waliominiwa na Tume kusimamia Uchaguzi ngazi ya Tume kujiamini, kujitambua na kuzingatia sheria na kanuni zote zinazotolewa na Tume ili kutenda haki na kufanya kazi kwa usahihi zaidi na hivyo kupelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kuwa salama na wa Amani.
Akiwa na imani na wateule hao, Mgeni rasmi amewaomba wasimamizi kutotumia uzoefu wa kusimamia Chaguzi mbalimbali zilizopita kwani uchunguzi unaonesha kuwa mazoea hupelekea kuharibu kazi badala yake wasikilize na kufuata kwa umakini mafundisho na maelekezo watakayopewa katika semina hiyo kutoka Tume.
Awali, Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndugu. Erasto Arende, aliwapongeza washiriki wote kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Tume kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ngazi ya Kata. Kikubwa amewataka kuonesha ushirikiano wa dhati katika zoezi hili kwa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo na wasimamizi wasaidizi ngazi ya Jimbo.
Semina hii imelenga kuwajengea uwezo wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata ili kutekeleza vyema majukumu yao katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi kuanzia sasa hadi viongozi wapya watakapopatikana. Semina itaendeshwa kwa muda wa siku tatu kuanzia leo tarehe 07/08/2020 hadi tarehe 09/08/2020.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda