Jumatatu 14.08.2023
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bwana Emmanuel Mkongo amesema hatomfumbia macho wala kumuonea huruma Mtendaji yeyote wa Kata atakae kwenda kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na hatasita kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu.
Aidha, amesema ni wajibu wa kila Mtendaji kufanya kazi kwa ufanisi, bidii na juhudi ili kuhakikisha majukumu yao yanatekelezwa kwa usahihi unaotakiwa.
Mbali na hayo, Mkurugenzi amewasisitiza Watendaji kushiriki Vikao na ziara mbalimbali za viongozi zinapokuwa zikifanyika katika maeneo yao ya kazi. Na pale inapotokea dharura basi itolewe taarifa katika mamlaka husika na kukaimisha nafasi hiyo.
Mkurugenzi amewaasa pia kuacha tabia ya kutopokea simu za Viongozi pindi wanapokuwa wanapigiwa na badala yake wapokee na kusikiliza maelekezo.
Mkurugenzi amewakumbusha pia kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata zao kwani wao ndio wasaidizi wake wakuu katika maeneo yao.
Mwisho Mkongo ametumia fursa hiyo kwa Watendaji wa Kata ya Bunda Stoo na Nyasura kupiga marufuku watu kuendelea kulima mpunga na mazao mengine katika maeneo yanayozunguka shule mpya za Msingi zinajengwa na badala yake maeneo hayo yatumiwe na wananchi kwa mujibu wa mipango miji iliyowekwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Ardhi, Mipango Miji na Mazingira.
Hayo yamesemwa leo katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kilicholenga kuwakumbusha Watendaji wa kata wajibu wao kazini.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda