Mheshimiwa Joshua Nassari Mkuu wa Wilaya ya Bunda amezindua rasmi miongozo iliyoandaliwa na Serikali kumsaidia Mwalimu na Mwanafunzi kufundisha na kujifunza na kisha kupata matokeo mazuri.
Akizindua Miongozo hiyo Mheshimiwa Nassari amesema" Changamoto za kufundisha na kujifunza zinatofautiana na namna ya kuzitatua ni tofauti hivyo miongozo hii isiwe kama Biblia au Msaafu kwamba kama ilivyoandikwa lazima iwe hivyo, mazingira yanatofautiana na miongozo hii imendaliwa kutumika Nchi nzima hivyo lazima Mwalimu awe mbunifu kuongezea mbinu mbalimbali pale zinapohitajika."
Mheshimiwa Nassari ameongeza kusema kuwa "Kila mtu apitie vizuri miongozo hii kwani itasaidia kujenga kujiamini katika kazi zetu kwasababu unawezakuta ulichokua unakifanya kwa uoga ukakikuta kwenye muongozo hivyo kikakufanya kujiamini zaidi. Lakini mwisho kinachopimwa ni matokeo mazuri, hivyo Mwalimu unaweza ukatumia mbinu mbalimbali halali kuhakikisha unapata matokeo mazuri."
Aidha, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya amewakumbusha Maafisa Elimu pamoja na Wakuu wa shule kuanza kujiandaa kutekeleza mradi unaotarajiwa kuja wa ujenzi wa madarasa kama alivyosikika Mheshimiwa Inocent Bashungwa na kulielekeza moja kwa moja kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Mheshimiwa Nassari amesema "Mwaka jana tulifanya vizuri lakini mwaka huu tufanye vizuri zaidi kwasababu muda wa utekelezaji utakuwepo wa kutoshakuhakikisha tunajenga vyumba vya madarasa vilivyo bora.
Awali Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mwalimu Saidi Ramadhani wakati akiwatambulisha wajumbe waliomo ukumbini alisema kuwa "Lengo la kusanyiko hili ni uzinduzi wa hii miongozo ambayo tayari tumeshaanza kuifanyia kazi katika maeneo yetu, hivyo tuhakikishe tunatimiza malengo kadri jinsi miongozo inavyoelekeza. Afisa Elimu amesema kuwa lengo la miongozo hii ni kuboresha Ufundishaji na ujifunzaji katika maeneo yetu na hatimae ufaulu uwe bora.
Uzinduzi huu umefanyika Kiwilaya na wajumbe toka Halmashauri zote mbili za Bunda walikuwepo, Halmashauri ya Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda