Jumla ya madarasa 48 ya shule za Sekondari 15 za Halmashauri ya Mji wa Bunda yaliyojengwa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa yamepokelewa na kuzinduliwa rasmi leo tarehe 15/01/2022 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Bw. Salumu Mtelela kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda.
Katibu Tawala amemshukuru na kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za ujenzi wa madarasa hayo ambayo yatachangia kuboresha elimu nchini.
Katibu Tawala ameeleza kuwa licha ya changamoto zilizokuwa zikijitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi lakini Uongozi ulipambana kuhakikisha kazi inaendelea. Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndugu Emmanuel J. Mkongo kwa ubunifu na kujiongeza kupitia mradi huu kujenga Ofisi 30 zenye uwezo wa kubeba walimu 8 katika shule zote za Sekondari zilizotekeleza mradi huu.
Mheshimiwa mgeni rasmi hakusita kutoa wito kwa walimu kuhakikisha wanayatunza madarasa hayo ili kuhakikisha yanadumu katika ubora wake. Pia amepongeza ubunifu wa Ofisi ya Mkurugenzi kuzalisha tofali zenye ubora kutoka katika kiwanda cha Halmashauri ya Mji wa Bunda ambazo zilitumika kujenga madarasa yote hamsini na tisa (59) yaliyojengwa kupitia mradi huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mhe. Michael Kweka, amesema ushirikiano mzuri baina ya Mkurugenzi, Wataalam, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu, Kamati za Ujenzi, Mafundi na Waheshimiwa Madiwani ndio silaha kubwa iliyowezesha kukamilisha ujenzi huu kwa kiwango kinachostahili.
Aidha, Mwenyekiti amezipongeza Kamati za Ujenzi za Shule chini ya Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kwa kusimamia vyema mradi huu.
Wakati huo huo Mheshimiwa Mwenyekiti ametoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo nchini hasa kwa kuleta fedha za ujenzi wa madarasa hayo.
Kwaniaba ya Waheshimiwa Madiwani wote Halmashauri ya Mji wa Bunda, Diwani wa Kata ya Kabarimu Mheshimiwa Mhona Nyahimbu ametoa pongezi kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na Kamati zake za ujenzi kwa kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo katika Kata zote 14 za Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndg. Emmanuel Mkongo ameeleza kwamba Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.18 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hamsini na tisa (59) kwa shule 15 za Sekondari na shule za Msingi Shikizi tatu. Mkurugenzi ameeleza kuwa hadi leo tarehe 15/01/2022 jumla ya madarasa 48 yamekamilika kwa asilimia 100 na madarasa 11 yaliyosalia yapo katika hatua za ukamilishaji ambapo yatakamilika ndani ya siku 7 zijazo. Aidha kupitia mradi huu Halmshauri imefanikiwa kujenga Ofisi 30 kwa shule zote zilizotekeleza mradi huu, kuweka vigae vyenye ubora kwa kila darasa pamoja na viti na meza 50 kwa kila darasa kwa shule za Sekondari.
Mkurugenzi ameeleza zaidi kuwa mradi huu umechangia kutoa ajira 748 kwa wananchi mbalimbali wakiwemo mafundi. Mkurugenzi ameongeza kwa kusema kuwa mradi huu utasaidia kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wote kwa mkupuo mmoja.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda