Ukiona vyaelea jua vimeundwa, Ukiona matokeo mazuri ya wanafunzi jua kuna jasho la Walimu nyuma yake. Katika kuendelea kuhakikisha shule ya Sekondari Bunda inaendelea kuboresha matokeo ya wanafunzi, Leo Uongozi wa shule umeendeleza Utamaduni wake wa kutambua na kuthamini nguvu na mchango mkubwa wa Walimu wake.
Chini ya Uongozi wa Mkuu wa shule Mwl. Charles Somba ametoa Zawadi ya Majiko ya gesi 49 ambapo kila mtumishi wa shule ambaye amechangia kwa namna Moja ama nyingine matokeo mazuri amezawadiwa jiko la gesi. Hii inajumuisha Walimu (Waliojiriwa na wanaojitolea), Wapishi, Walinzi, Nesi wa shule pamoja na Mwandishi Mwendesha Ofisi (OMS).
Mbali na Zawadi ya Majiko, Walimu waliofanya vizuri katika masomo yao kwa kuzingatia madaraja ya ufaulu ikiwemo kufuta kabisa daraja F wamepewa fedha taslimu kama Motisha ya kuendelea kufanya vizuri. Jumla ya fedha taslimu Shilingi milioni 3.29 zimetolewa.
Akikabidhi zawadi hizo katika tafrija fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Heriet Mwl. Ayubu H. Mbilinyi Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mara ambaye pia alikua Mgeni Rasmi akimwakilisha Afisa Elimu Mkoa wa Mara ameupongeza Uongozi wa shule ya Sekondari Bunda kwa kutambua mchango wa Walimu katika kufanikisha matokeo mazuri ya wanafunzi kwa kutoa Motisha nzuri inayowapa moyo na hamasa Walimu kuendelea kufanya vizuri zaidi
Wageni wengine walioalikwa ni Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Mji wa Bunda Mwl. Christopher Katega akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Manyara Mwl. Kora Machota, Idara ya Elimu Sekondari ikiwakilishwa na Madam Sauda Mwakyembe, Afisa Elimu Kata ya Kabarimu pamoja na Wakuu wa shule za Sekondari za Halmashauri ya Mji wa Bunda wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wakuu wa shule (TAHOSA) Mwl. Bwire.
Shule ya Sekondari Bunda imefanikiwa kwa asilimia 100 kuondoa daraja sifuri katika matokeo ya Kidato Cha nne. Kwa mwaka 2023 matokeo ya kidato Cha nne yalikua kama ifuatavyo Daraja I - 29, II -38, III - 37, IV - 66, 0 - HAKUNA
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda