Mhe. Joshua Nassari Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Leo tarehe 08/11/2021 ametembelea miradi wa ujenzi wa madarasa unaondelea katika Halmashauri ya Mji wa Bunda kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO – 19 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Sekondari ya Wariku, Nyiendo na shule ya Shikizi ya Ligamba B.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kupitia Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa Bodi na kamati za shule za shule ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi hiyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita. Mhe. Nassari ameeleza kuwa ushiriki huu sio wa kutoa fedha bali kushiriki katika shughuli mbalimbali kama kuchimba msingi, kubeba maji, mchaga na mambo mengineyo kulingana na asili ya eneo husika. Mfano mzuri wa ushiriki wa wananchi umeonekana katika Shule ya Msingi Shikizi ya Ligamba B ambapo wananchi wameshiriki katika kuchimba msingi, kusomba mawe na kubeba mchanga. Juhudi hizi zitasaidia katika kuokoa fedha ambazo zinaweza kutumika kukamilisha mambo mengine shuleni.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amewaekelekeza Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti, Watendaji wa kata na mitaa na Uongozi wa shule kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atakaekwamisha ujenzi wa madarasa hayo. Mhe. Nassari amewataka walimu kuendelea kufundisha na kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa madarasa kupitia kamati zilizoundwa kwa utaratibu wa “Force Account” katika shule hizo.
Katika kuhakiksha ujenzi huu wa madarasa unakwenda kama ilivyopangwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndg. Emmanuel Mkongo amemhakikishia Mhe. Mkuu wa Wilaya kwamba upatikanaji wa tofali zilizo bora na viwango kwa shule zote upo na kwamba tofali zote zitazalishwa katika kiwanda cha Tofali cha Halmashauri ili kudhibiti ubora ambapo hadi sasa kiwanda kinaendelea kuzalisha tofali hizo. Mkongo ameeleza kuwa Serikali imeelekeza Halmashauri kuratibu ununuzi wa vifaa vya ujenzi, mabati, mbao, na saruji kuagizwa kwa pamoja (Bulk procurement) ili kupunguza gharama. Hata hivyo, Halmashauri inaendelea kufanya upembuzi wa utengenezaji wa viti na meza pamoja na madawati kwa pamoja ili kupunguza usumbufu kwa walimu unaoweza kujitokeza wakati wa utengenezaji wa leja leja.
Halmashauri ya Mji wa Bunda imepokea Jumla ya shilingi Bilioni 1.8 kwaajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO – 19 ili kutekeleza Miradi ya ujenzi wa vyumba 51 vya madarasa ya shule za sekondari na vyumba vya madarasa 8 vya shule za msingi.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda