Saturday 18th, January 2025
@BUTAKALE KATA YA BUNDA STOO
HALMASHAURI YA MJI WA BUNDA
UZINDUZI WA ZOEZI LA UPIGAJI CHAPA MIFUGO (NG’OMBE)
Halmashauri ya Mji wa Bunda, imezindua zoezi la upigaji chapa mifugo (ng’ombe) katika Kata ya Bunda Stoo, mtaa wa Butakare na Migungani tarehe 07/09/2017, uzinduzi ambao ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh. Lyidia Bupilipili.
Mkuu wa Wilaya aliwapongeza wafugaji na wananchi wote waliojitokeza kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi huo na wale ambao walileta ng’ombe kwa ajili ya kupigwa chapa.
Mkuu wa Wilaya aliwaasa kutopuuzia zoezi hilo kwa kuwa ni agizo la Serikali, hivyo ni lazima kila mfugaji ahakikishe ng’ombe wake wote wamepigwa chapa na si vinginevyo, alisisitiza kwamba kwa zoezi la upigaji chapa wafugaji watapumzika na adha za wizi wa mifugo kwa sababu ng’ombe watakuwa wanatambulika kila watakapopita kuwa ni ng’ombe wa eneo fulani.
Pamoja na uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya aliwataka wafugaji wote wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kutobweteka na kumiliki makundi makubwa ya mifugo wakati sifa za mji haziruhusu kutenga maeneo ya malisho, kinachotakiwa ni kuvuna mifugo yao mara kwa mara na kufanya shughuli zingine za maendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga shule za sekondari kwa ajili ya watoto wao, aliwakumbusha kuwa Kata yao haina shule ya sekondari, hivyo badala ya kutafuta eneo la malisho ya mifugo yao, wahakikishe eneo la kujenga shule linapatikana, baada ya hapo wavune mifugo hiyo na kujenga shule na sio kuwatembeza watoto wao na fimbo tu bila kuwaendeleza kielimu.
Akiongea kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bi Janeth Peter Mayanja, pamoja na juhudi za wafugaji za kuungana na Serikali kuhakikisha kwamba zoezi hilo linafanikiwa baada ya wataalam wa mifugo kuwaelimisha, aliwaambia faida zingine za upigaji chapa ni pamoja na kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji, udhibiti wa magonjwa ya mifugo na kuimarisha biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi, pia Serikali itakuwa na nafasi ya kukaa na kuongea na wafugaji katika kupanga mipango ya uendelezaji mifugo kwa kuwa mifugo yao itakuwa imesajiliwa na kutambuliwa tayari kwa ajili ya kuhudumiwa.
Awali katika taarifa yake kabla ya uzinduzi wa zoezi hilo, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bwn Rick Stevens Kaduri alisema, Halmashauri ina lengo la kupiga chapa ng’ombe 77,394 katika Kata zote 14 ambapo kutakuwa na vituo 36, gharama zinazotarajiwa kutumika ni Tsh. 11,850,000.00 (milioni kumi na moja na laki nane na hamsini tu), fedha hizo ni pamoja na gharama za uhamasishaji (mikutano na matangazo), kutengeneza chapa pamoja na nguvu za wananchi.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda