Leo tarehe 22/11/2021 Halmashauri ya Mji wa Bunda imefanya Mkutano wa Baraza la Halmashauri ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Baraza la kuwasilisha ya Taarifa za Kata uliofanyika tarehe 18/11/2021 ambapo Taarifa za Kata tano za Balili, Kabarimu, Kunzugu, Bunda Mjini na Guta ziliwasilishwa na kujadiliwa na Waheshimiwa Madiwani.
Katika siku ya pili ya Baraza chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Michael Kweka, imeelezwa kuwa Halmashauri itatoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ndani ya mwezi Novemba ambapo vikundi vilivyotakiwa kupewa mikopo kipindi kilichopita vitapewa kipaumbele.
Baraza pia limeazimia Kamati ya Kudumu ya Halmashauri ya Mipangomiji na Mazingira kwenda kutembelea maeneo ambayo yamependekezwa na Kamati ya wataalamu kujenga Hospitali ya Halmashauri ambayo ni kata ya Guta, Bunda stoo na Sazira. Baada ya kutembelea, Kamati imetakiwa kuleta mapendekezo ambayo yatajadiliwa na kupitishwa katika Baraza lijalo la Mwezi Januari, 2022.
Aidha, Kupitia Mkutano huu Waheshimiwa Madiwani wamepitia, kujadili na kuridhia mapendekezo ya Sheria Ndogo za Usafi wa Mazingira zilizopitishwa na Baraza lililopita la Madiwani ili kuhuishwa na kupelekwa kusainiwa na Waziri Mwenye Dhamana. Rasimu ya Sheria Ndogo ilirudishwa kutokana na mabadiliko ya Uongozi yaliyofanyika katika Ofisi ya Rais TAMISEMI na Halmashauri.
Katika Mkutano huo, Taasisi za Serikali zilizoalikwa zilipata nafasi ya kuwasilisha taarifa za utekelezaji.
Kwa upande wa TARURA, ilielezwa kuwa barabara zinazofanyiwa ukarabati kwa sasa zinatokana na bajeti iliyopitishwa ya mwaka 2021/2022.
Aidha, Waheshimiwa Madiwani wamemtaka Meneja wa TARURA kushirikiana nao kubaini barabara zenye changamoto na kuzifanyia kazi.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Bunda (BUWSSA) alieleza kuwa changamoto za maji zinazotokea kwa wakati huu zinatokana na matengenezo ya barabara ya Bunda – Serengeti, hali iliyopelekea mabomba mengi kukatwa. Hata hivyo, Kaimu Meneja amefafanua kuwa changamoto hizo zimeanza kutatuliwa na muda si mrefu huduma ya maji itarudi katika hali ya kawaida.
Kuhusu shilingi milioni 500 zilizotolewa na Serikali kutatua changamoto ya maji katika Kata ya Kabasa mtaa wa Bitaragauru, Meneja wa RUWASA ameeleza kuwa tayari fedha hizo zimepokelewa na utekelezaji utaanza mara moja.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda