Tarehe 07.09.2022
Leo Baraza la Halmashauri ya Mji wa Bunda robo ya nne limefanyika chini ya Mheshimiwa Mwenyekiti Michael Kweka.
Kamati nne zimewasilisha taarifa za utekelezaji wa kazi kwa kipindi Cha robo ya nne ambazo ni Kamati ya kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya, Kamati ya Mipango Miji na Mazingira na Kamati ya Fedha na Utawala. Wajumbe wa Baraza walipata nafasi ya kujadili na kutoa maoni kwa Kamati hizo ambayo kwa hakika yalilenga kuijenga Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Baadhi ya mambo ambayo Baraza imeyaeleza ni eneo la makaburi na dampo kuwekwa alama za kudumu Ili kuepusha uvamizi wa watu katika eneo Hilo.
Aidha Baraza limeeleza juu ya mikopo ya vikundi kwa vikundi vyote ambavyo viliidhinishiwa mikopo lakini havikupata fedha na vingine kupewa nusu kwamba vikundi Hivyo vitapewa kipaumbele katika mikopo itakayotolewa katika robo ya kwanza na tayari vikundi Hivyo vimeshaanza mchakato wa kujisajili na mfumo mpya Ili viweze kupewa mikopo hiyo.
Baraza limeeleza pia kuhusu uchakachuaji wa utengenezaji wa matofali uliojitokeza katika Kiwanda Cha Halmashauri ya Mji wa Bunda na kusema kuwa Halmashauri ilipata Taarifa hiyo na tayari hatua za kisheria na kinidhamu kwa wote waliohusika zinaendelea dhidi ya watu hao.
Kuhusu Miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Baraza imeeleza kuwa ni wajibu wa kila Diwani kusimamia Miradi hiyo Ili itekelezwe katika ubora unaohitajika. Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bw. Emmanuel Mkongo amesema kwamba fedha zote zitakazokuwa zinapelekwa katika Miradi Waheshimiwa Madiwani watakua wanapewa taarifa ili kuongeza usimamizi.
Mwisho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bw. Emmanuel Mkongo alitoa taarifa kwa wajumbe kwamba Halmashauri imeshika nafasi ya Saba kati ya Halmashauri 184 zilizofanya vizuri katika utendaji kazi na usimamizi mzuri wa kuwahudumia Wananchi. Mkurugenzi ameongeza kusema kuwa mafanikio hayo yamekuja kutokana ushirikiano mzuri uliopo baina ya watendaji na Waheshimiwa Madiwani Hivyo kuomba kudumisha Umoja huo na kuendelea kuwatia moyo Watendaji.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda