Wanachama wa vyama vya kuweka na kukopa mkoani Mara wameshauriwa kuwa wakweli na waaminifu katika kurejesha mikopo yao ili kudumisha uhai wa Saccos zao.
Mkuu wa mkoa wa Mara Bw. Adam Kighoma Malima ametoa rai hiyo katika viwanja vya Ofisi za Halmashauri ya mji wa Bunda wakati akizindua Saccos wa wanawake wa mji wa Bunda (BTW Saccos) ambayo ni chama cha kuweka na kukopa cha wajasiriamali wanawake.
Bw. Malima ambaye katika uzinduzi huo alifuatana na viongozi mbalimbali, pia amewaasa wanawake na wananchi mkoani Mara kutumia fursa zilizopo kujijenga kiuchumi. Aidha ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wazazi na wananchi kwa ujumla wao kutokomeza kabisa unyanyasaji wa mtoto wa kike.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mbunge wa viti maalum Mh. Agnes Marwa amewapongeza wanawake wa halmashauri ya mji wa Bunda kwa kuamua na kutubutu kuanzisha chama cha kuwajenga kiuchumi na kusisitiza kuwa tarehe 10 Januari 2018 ndiyo mwanzo wao kuwa huru kiuchumi. Vilevile Mh. Marwa ameomba kujiunga na chama hiki cha kuweka na kukopa cha BTW.
Zaidi ya Sh 26,500,000 ziliahidiwa kutunisha mfuko wa Saccos hiyo, Benki ya posta milioni 10, Mbunge Mh. Marwa milioni 6, na Ofisi ya mkuu wa Mkoa laki 5,ambapo Mh. Marwa aliahidi kuchangia kiwanja chenye thamani ya Sh milioni 4.
Mapema Mkurugenzi wa mji wa Bunda Bi. Janeth P. Mayanja alisema kuwa wameanzisha Saccos hiyo ili kuwawezesha wajasiriamali nchini, hususani wanawake, ili kuondoa umaskini wa pato.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda