Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Bwn. Emmanuel Mkongo ameishukuru Timu nzima ya TWENDE BUTIAMA kwa kuichangia shule ya Msingi Nyerere Madawati 70 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5 pamoja na kutoa miti 1,000 itakayopandwa katika shule hiyo ikiwa ni moja ya kampeni yao ya Twende Butiama.
Msafara wa Twende Butiama ulianza safari ya kuendesha Baiskeli kutoka Jiji la Dar es salaam kuelekea Butiama ambapo leo umefika katika Wilaya ya Bunda hususani katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na kuweka kambi katika shule ya Msingi Nyerere.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mkongo ameishukuru Timu ya Twende Butiama kwa heshima waliyoipatia Wilaya ya Bunda kwa kuwa sehemu ya Malengo ya Twende Butiama. Aidha, Mkongo amewasihi kuendelea kudumisha fikra za Mwalimu Nyerere za kudumisha Upendo, Umoja na Amani na kuendelea kupambana na maadui watatu ambao ni Ujinga, Maradhi na Umasikini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Twende Butiama Bwn. Gabreil Landa amesema kwamba Twende Butiama imefikisha miaka mitano toka kunzishwa kwake mwaka 2019 na malengo yake makuu yakiwa matatu ambayo ni kudumisha Amani, Umoja, mshikamano na Upendo, Pili, Elimu kwa kuhamasisha Watanzania kuchangia katika Elimu na Mwisho Suala la Mazingira kwa kuhamasisha Wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, Mwenyekiti wa Msafara amesema tangu waanze msafara huo wa kwenda Butiama wameshatoa zaidi madawati 300 katika maeneo yote waliyopita ambapo kwa shule ya Msingi Nyerere wametoa madawati 70.
Twende Butiama imekua na wadhamini mbalimbali ambapo mdhamini mkuu kwa mwaka 2023 ni Kampuni ya vodacom ambao wamesaidia kupatikana kwa madawati hayo pamoja na miti 1,000 ya kupandwa.
Awali katika Risala yake, mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyerere Edwine Byangwamu ameishukuru kampeni ya Twende Butiama ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana katika shule hiyo. Msafara wa Twende Butiama leo ni mara ya tatu wanafika shule ya Msingi Nyerere na kufanya matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja kupanda miti.
Bunda Town Council
Anuani ya Posta: 219 Bunda
Sim: +255 28 2621773
Mobile:
Barua Pepe: info@bundatc.go.tz
haki zote zimehifadhiwa.Haki miliki ©2017 Halmashauri ya mji wa bunda